Dodoma FM

Mchakato wa Mabadiliko Yanga wafikia pazuri

2 December 2020, 10:51 am

Injinia Hersi Said na Alvaro Paya mwakilishi wa La Liga

Dar es Salaam.

Meneja wa mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu ya Yanga SC,injinia Hersi Said akiambatana na kamati ya Mabadiliko ya Yanga, leo Jumatano Desemba. 2, 2020 wamekabidhi rasimu ya awali ya mchakato wa mabadiliko kwa uongozi wa Yanga.

Hivi karibuni Mkurugenzi wa Uwekezaji kutoka kampuni ya GSM Injinia. Hersi Said na Alvaro Paya mwakilishi wa La Liga walielekea nchini Hispania kwa ajili ya kukabidhiwa rasmi rasimu ya awali ya uendeshwaji wa klabu.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam hii leo, Mwenyekiti wa Yanga, Dkt.Mshindo Msola amesema kuwa kuna karatasi 400 ambazo zimezungumza kuhusu mchakato huo ambao utaleta mabadiliko ndani ya klabu hiyo kwa kufuata sheria za Serikali.

Msola amesema walipaswa kufanya mkutano hivi karibuni ila walighairi kwa ajili ya mchakato huo ambapo leo makabidhiano ya rasimu hiyo imefanyika huku uongozi ukiwa umeanza kuandaa mpango kazi kwa ajili ya mkutano mkuu utakaoitishwa  hivi karibuni.

Mshauri kwenye masuala ya mabadiliko, Senzo Mbatha amesema kuwa anaamini kwamba kila kitu kitakuwa sawa na watafikia malengo ambayo wanayahitaji.