Dodoma FM

Micho akana mashtaka A.Kusini

12 December 2020, 10:42 am

Milutin Micho

Johanesburg,

Afrika Kusini.

Kocha Mkuu wa Timu ya taifa ya Zambia Milutin Sredojevic ‘Micho’ amekana mashtaka ya unyanyasaji wa kijinsia nchini Afrika Kusini.

Kocha huyo mkongwe barani Afrika, mwenye umri wa miaka 51 alipandishwa katika Mahakama huko New Brighton jana Ijumaa kabla ya kuachiliwa kwa dhamana ya R10,000 ($660/Tshs 1.5m).
Tuhuma za Micho zitasikilizwa tena mnamo Februari 25 mwakani. Inadaiwa kuwa visa viwili vilitokea mnamo Disemba 7 wakati wa Michuano inayoendelea ya Kombe la Vijana chini ya miaka 20 la COSAFA kwenye Uwanja wa Wolfson huko Port Elizabeth; Vikimuhusisha Micho na Mwanamke Mmoja Ambaye Alikuwa akimletea Kahawa.
“Hizi ni shutuma zisizo na msingi zilizokusudiwa kuikandamiza timu ya Zambia ambayo haijafungwa goli kwenye mashindano haya (Kombe la Cosafa chini ya miaka 20),” Sredojevic amenukuliwa na BBC.
“Wawakilishi wangu wa kisheria wanashughulikia suala hili”.
Msemaji wa Mamlaka ya Mashtaka ya taifa, Anelisa Ngcakani alisema Micho ameachiwa kwa dhamana ya R10 000, na kesi hiyo iliahirishwa hadi 25 Februari 2021; Kwa Mujibu wa Ngcakani, Micho aliulizwa na Mwanamke huyo mwenye Umri wa Miaka 39 Kama atahitaji Kahawa na Sukari yake.