Dodoma FM

80 wakosa masomo Chamwino kwa uhaba wa madarasa

17 February 2021, 1:31 pm

Na, Benard Filbert,

Dodoma.

Zaidi ya wanafunzi 80 wa kidato cha kwanza mwaka 2021 wameshindwa kuripoti shuleni, kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa uliyopo katika shule ya Sekondari Membe Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma.

Hayo yameelezwa na Diwani wa Kata hiyo Bw.Simon Macheo wakati akizungumza na taswira ya habari ambapo amesema kuwa shule ya Secondari Membe ina upungufu wa madarasa matatu hali inayochangia idadi kubwa ya wanafunzi kidato cha kwanza kutokuripoti shule mpaka sasa.

Bw.Macheo amesema mwaka jana kulikuwa na chumba kimoja kwa ajili ya maabara ambacho baadae kilibadilishwa matumizi yake na kutumika kama darasa.

Ameongeza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino imeleta baadhi ya vifaa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa shule hiyo lakini bado havikidhi mahitaji.

Jumla ya Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Membe 2021 ni 143, na walioripoti mpaka sasa ni 50 pekee huku wengine wakisubiri hadi kumalizika kwa madarasa mengine.