Dodoma FM

Idadi ya wanaume wanaopima VVU yaongezeka

9 March 2021, 12:56 pm

Na, Yussuph Hans, – Dodoma.

Imeelezwa kuwa kupitia mkakati wa Serikali wa kumtaka mama mjamzito kuambatana na mwenzi wake kliniki umesaidia kwa kiasi kikubwa kuwapima virusi vya ukimwi wanaume ambao awali,walikuwa wagumu kupima.

Hayo yamebainishwa na mratibu wa Ukimwi kwenye idara ya maendeleo ya jamii Bi.Daisy Nabo, wakati akizungumza na taswira ya habari juu ya njia zinazotumika kuhamasisha wanaume kujitokeza kupima Virusi vya Ukimwi ambapo kundi hilo ndilo linaloonekana kuwa nyuma katika upimaji.

Ameongeza kuwa mkakati huo umekuwa na mafanikio makubwa, pamoja na kuandaa mabonaza ya michezo inayowashirikisha watu wa rika mbalimbali ambapo wataalamu hutumia fursa hiyo kuwapima kwa hiyari wanapojitokeza katika mabonanza hayo.

Sanjari na hayo Taswira ya habari imezungumza na vijana jijini Dodoma juu ya sababu zinazowapa hofu wanaposhauriwa kupima afya zao, ambapo wamesema ukosefu wa elimu ya kina kuhusu maambukizi ya VVU ndio changamoto kubwa.

Kwamujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya kudhibitibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dr. Leonard Maboko, takwimu za mwaka 2019 zilionesha kuwa wanaume wanaoishi na VVU nchini walikua 628,830, huku wanawake wakiwa ni 983,471 lakini vifo vinavyotokana na ugonjwa huo kwa Wanaume ni 12,225 huku Wanawake ni 9,304.