Dodoma FM

Hatimaye zoezi la kumuaga Dkt John Magufuli lahamia Dodoma

21 March 2021, 1:57 pm

Na; Mariam Kasawa

Wakazi wa Mkoa wa Dodoma na maeneo ya jirani wametakiwa kujitokeza mapema katika uwanja wa Jamhuri kwaajili ya kushiriki zoezi la kumuaga hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Akizungumza na waandishi wa habari Msemaji mkuu wa Serikali Dkt.Hassani Abbas amesema zoezi la kuaga litaanza mapema asubuhi ambapo litaanzia Bungeni ili kuwapa fursa wabunge waweze kumuaga Hayati Rais Magufuli na baada ya hapo zoezi hilo litahamia uwanja wa jamuhuri ambapo viongozi mbalimbali pamoja na  wananchi watapata fursa ya kuaga.

Aidha Dkt. Abbas amesema zoezi hilo litahudhriwa na Marais wa Nchi nyingine 11 pamoja na wawakili  wapatao 50 ambapo amewataja Marais watakao hudhuria  kuwa ni  pamoja na.

 Rais Uhuru Kenyata wa Kenya, Rais Razarius Chakwale wa Malawi, Rais Azali Assouman wa Comoro, Rais Philipe Nyusi wa Msumbiji, Rais Emmason Mnangagwa wa Zimbabwe, Rais Edger Rungu wa Zambia, Rais Hage Gengbo wa Namibia, Rais  Mokgweetis Masis wa Botswana, Rais Cyril Ramaphosa wa  Afrika Kusini, na  Rais Felix Tshiseked wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo .

Sanjari na hayo amewataja viongozi watakao wawakilisha Marais wao kuwa ni pamoja na Waziri Mkuu wa Rwanda, Waziri wa Mambo ya nje wa Angola,  Makamu wa Rais wa Burundi, pamoja na viongozi mbalimbali kutoka asasi za kikanda ikiwemo SADC, Umoja wa Mataifa ofisi ya Tanzania.

Pia amesisitiza kuwa kesho Machi 22 itakuwa siku ya mapumziko na Machi 26 siku ya maziko pia itakuwa siku ya mapumziko Kitaifa.

Dkt .Abbas amewataka wananchi kujitokeza barabarani kwa wingi wakati mwili wa Rais Magufuli utakapo kuwa unawasili mjini Dodoma pia amewasihi wananchi kuendelea kuliombea Taifa la Tanzania pamoja na Kumuombea Hayati Dkt John Pombe Magufuli apumzike kwa amani.