Dodoma FM

Magufuli Alijenga Heshima ya Tanzania

23 March 2021, 6:34 am

Na; Mariam Kasawa.

Imeelezwa kuwa, kufuatia Marekebisho yaliyofanywa katika Sheria ya Madini ambayo ni Matunda ya jitihada za aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli yameifanya  Tanzania iheshimike kimataifa.

Hayo yamebainishwa Machi 22, 2021 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi alipokuwa akitoa Wasifu wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Marekebisho na Sheria ya Madini yaliyokuwa yakisisitizwa na aliyekuwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli yameifanya Tanzania kunufaika na rasilimali zilizopo Nchini humo.

Aidha, Prof. Kabudi amesema kukamilika kwa ujenzi wa Ukuta unaozunguka Migodi ya Tanzanite  na Mirerani, umesaidia kudhibiti utoroshwaji wa Madini ya Tanzanite ambapo kwa sasa ulinzi wake umeimarika na hivyo kuongezeka kwa mapato yatokanayo na madini hayo.

Prof. Kabudi amesema, Rais Magufuli kwa ujasiri na uthubutu wake amesaidia kuhakikisha Serikali inapata asilimia 16 za hisa kutoka kwa wawekezaji wanaochimba  madini nchini  lengo likiwa kufikia asilimia 50 jambo ambalo ni la kizalendo kwa nchi yake.

Amesema, kutokana na maelekezo ya Hayati Dkt. Magufuli, yalianzishwa masoko kila Mkoa ambayo yameongeza ukusanyaji wa Mapato ya Serikali yatokanayo na Rasilimali Madini.

Naye, Uhuru Kenyata, Rais wa Kenya amesema, Hayati Magufuli amesaidia kwa kiwango cha juu kuhakikisha Tanzania haitegemei msaada kutoka nje ya Nchi na badala yake alihakikisha rasilimali zilizopo nchini zinatumika katika kuiletea maendeleo Tanzania.