Dodoma FM

Vyombo vya ulinzi na usalama vitamtii Rais Samia

26 March 2021, 11:23 am

Na; Mariam Kasawa

Mkuu wa Majeshi  nchini Tanzania (CDF) Venance Mabeyo amemuhakikishia Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania mama Samia Suluhu Hassan kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vitamtii na kutekeleza majukumu yake kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania..

Akizungumza katika ibada ya mazishi ya Rais wa Awamu ya Tano Hayati John Magufuli leo Ijumaa Machi 26, 2021 wilayani Chato Mkoani Geita kwa niaba ya Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama,  Mabeyo ameeleza kuwa hali ya Nchi ni shwari na wataendelea kuimarisha ulinzi.

Amesema ulinzi wa Nchi na mipaka yake ni salama na vyombo vitaendelea kumlinda Rais, kumtii kama Amiri Jeshi Mkuu na kutekeleza majukumu  kama ilivyoainishwa kwenye katiba.

Mabeyo ametumia fursa hiyo kumualika Rais Samia kuwatunuku nishani askari wanafunzi waliotakiwa kutunikiwa nishani hizo Machi 10, 2021.

Amesema vyombo hivyo vitaendelea kuonyesha uadilifu, utiifu na uaminifu kwake kama ilivyokuwa kwa awamu za uongozi zilizopita.