Dodoma FM

Wasichana wahimizwa kutambua umuhimu wa masomo ya Sayansi

12 April 2021, 11:33 am

Na; Yussuph Hans

Licha ya uhaba wa Wanafunzi wa Kike kusoma Masomo ya Sayansi Nchini, bado kuna changamoto mbalimbali zinazowakabili baada ya kuhitimu Masomo hayo.

Hayo yamebainishwa na Afisa Mpango Ujenzi wa Nguvu za pamoja na harakati kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania, Flora Ndaba wakati akizungumza na taswira ya habari juu ya chanzo kinachosababisha kuwepo kwa uhaba wa wanafunzi wa kike katika masomo ya sayansi.

Bi.Flora amesema kuwa moja ya jukumu kubwa wanalolifanya kwa sasa ni kueneza uwazi kwa wasichana kutambuwa umuhimu wa masomo hayo licha ya wanafunzi wengi kuacha kuchagua masomo ya Sayansi wafikapo shule za upili.

Aidha amesema pia kumekuwa na mwamko mdogo kwa wanafunzi wa kike kusomea ufundi na pindi wanapohitimu masomo hayo hujishughulisha na biashara mbadala badala ya kutumia taaluma zao.

Taswira ya habari imezungumza na Mwalimu Paul Ezekiel pamoja na wanafunzi waliosomea fani mbalimbali katika Chuo Cha Ufundi VETA Dodoma, ambapo wamesema changamoto kuu ni ushawishi katika kazi pamoja na wengine kuacha kutumia taaluma zao baada ya kuingia katika maisha ya ndoa.

Sanjari na hayo Mwalimu Ezekiel amewashauri wanafunzi wa kike kujituma katika taalumu za ufundi wanazosomea ili kujikomboa katika wimbi la ukosefu wa Ajira.