Dodoma FM

Wadau wa mazingira waipongeza Serikali kwa hatua ya kutokomeza mifuko ya plastiki

16 April 2021, 11:13 am

Na; Mariam Matundu.

Wadau wa mazingira wanasema wanafurahi kuona jitihada zao za kutaka kutokomezwa matumizi ya plastiki zinaendelea kufanikiwa kutokana na athari zake katika mazingira.

Hayo yamesemwa na mdau wa mazingira kutoka taasisi ya Fudeco Bakari Mntembo na kuongeza kuwa walianza kupigia kelele suala hili tangu mwaka 2016.

Aidha amesema anasikitishwa kuona jitihada zinachukuliwa taratibu kwa kuwa bado kuna matumizi ya vifungashio vya plastiki.                        

Pamoja na hayo amesema wanamatumaini kauli ya waziri wa muungano na mazingira kuwaita wawekezaji ili wakutane Aprili 17 kujadili changamoto zinazokwamisha uzalishaji na usambazaji wa vifungashio mbadala watakuja na majibu sahihi.

Mapema wiki hii waziri mwenye dhamana ya muungano na mazingira mh Sulemani Jafo ametangaza kukutana na wawekezaji Aprili 17 baada ya kutokupatikana kwa vifungashio mbadala tangu zuio la matumizi ya vifungashio vya plastiki ambapo Aprili 9 ndio ulikuwa mwisho.

Utakumbuka mapema mwezi Januari zilitolewa Siku 90 kuhakikisha uzalishaji wa  vifungashio mbadala na kuzuia uzalishaji , usambazaji, na matumizi ya vifungashio vya plastiki ambavyo mwisho wa  matumizi yake ulikuwa ni Aprili 9 mwaka huu.