Dodoma FM

Chidilo walalamika kukosa huduma zitokanazo na nishati ya umeme.

22 April 2021, 10:56 am

Na; Victor Chigwada.

Imeelezwa kuwa kukosekana kwa huduma ya umeme katika Kijiji cha Chidilo Kata ya Mpalanga Wilayani Bahi kumechangia kwa kiasi kikubwa kakosekana kwa huduma nyingine zinazotegemea nishati hiyo.

Hayo yamebainishwa na baadhi ya wananchi wa Kijiji hicho wakati wakizungumza na Dodoma Fm ambapo wamesema umeme umepita barabarani lakini haujaunganishwa katika Vitongoji vya Kijiji hicho.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho  Bw.Marino Mgunda amesema umeme umefungwa kwa kufuata barabara huku ukiwa haujaunganishwa katika makazi ya watu.

Naye Diwani wa Kata ya Mpalanga Bw.Baraka Ndahani amesema  zoezi la usambazaji nguzo za umeme kwenye Vitongoji lilishaanza lakini kwasasa limesimama kutokana na changamoto mbalimbali za kiofisi.

Bw. Ndahani ameongeza kuwa zoezi hilo litakapoendelea asilimia kubwa ya vitongoji vyote vitanufaika na mpango huo huku taasisi za kidini na shule zikipewa kipaumbele.

Hata hivyo Serikali imejipanga kuhakikisha wakala wa umeme Vijijni REA unafikisha huduma hiyo katika Vijiji vyote vilivyopo kwenye mpango wa kupata umeme.