Dodoma FM

Ukosefu wa elimu ya Afya kwa mabinti ni sababu kubwa ya maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU)

3 May 2021, 10:29 am

Na; Mariam Matundu.

Imeelezwa kuwa ili kuongeza ufahamu kuhusu masuala ya afya ya uzazi  kwa vijana ni muhimu kuongeza wigo wa utoaji elimu hiyo pamoja na mazingira rafiki yanayomuwezesha kijana kupata elimu hiyo.

Debora Frenk ni afisa mradi wa EPIC unaojihusisha na utoaji wa afua mbalimbali kwa vijana balehe na wanawake vijana  kutoka FHI360 ,amesema ukosemu wa elimu ya afya ya uzazi kwa mabinti ni sababu mojawapo inayowaweka katika hatari ya kupata maambukizi ya  virusi vya ukimwi (vvu ).

Akizungumzia afua wanazozifanya ili kuwakomboa wasichana katika hatari ya kuambukizwa vvu amesema wamekuwa wakitumia waelimishaji rika kwa kuwajengea uwezo  na kuwawezesha  wao kwenda kuwaelimisha wengine.

Nae afisa mradi wa DREAMS kutoka FHI 360 mkoa wa Shinyanga Getrude Sebio amesema changamoto kubwa iliyopo kwa mabinti ni kutokujitambua na kujua thamani yao ambapo kupitia mradi huo wamefanikiwa kuwafikia mabinti elf 38 .

Nao baadhi ya mabinti walionufaika na mradi huo wamesema mradi huo umewaisaidia kuwajengea uwezo wa kujiamini ,kujitambua pamona na kupima vvu na kujua hali zao za kiafya na kwamba elimu hiyo wanaitumia kuwaelekeza mabinti wengine.

Kwa mujibu wa tume ya Taifa ya kudhibiti ukimwi Tanzania (TACAIDS) unasema  katika kila maambukizi mapya yanayotokea 40% ni vijana wa miaka 15 hadi 24 na miongoni mwao 80% ni wasichana.