Dodoma FM

Watoto wa kike wahamasishwa kupenda masomo ya sayansi

11 May 2021, 2:05 pm

Na; Mariam Matundu. 

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF), Justina Mashiba amesema kupitia miradi ya mfuko huo wamekuwa wakitoa mafunzo yenye lengo la kumuhamasisha mtoto wa kike kupenda masomo ya sayansi, kuwa mbunifu na kupenda kujifunza masuala ya teknolojia na TEHAMA awapo shuleni.

Amesema kuwa mpaka sasa UCSAF imetoa mafunzo ya TEHAMA kwa wanafunzi wa kike 744 wa shule za umma Tanzania nzima, imetoa vifaa vya TEHAMA kwa shule takribani 700 pamoja na kuunganisha shule 400 za umma na mtandao wa intaneti.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula amepongeza juhudi za UCSAF huku akitoa wito kwa  taasisi hiyo ya Serikali kuendelea kushirikiana na wadau wengine katika kuufanya ubunifu kuwa rafiki kwa wanawake na wasichana nchini.

Nae mbunge wa viti maalum CCM, kundi la Asasi za kiraia Tanzania Bara. Mhe. Neema Lugangira ametoa wito wa kupitia sera ili kuhakikisha zinamjumuisha msichana na mwanamke hasa aliyeko pembezoni huku akisisitiza kuwa wanawake wanaoishi maeneo ya vijijini wanapaswa kuwa na uelewa wa matumizi ya teknolojia zilipo.

Wadau mbali mbali wamekutana katika majadiliano hayo  yaliyoandaliwa na kituo cha ujasiliamali na ubunifu cha Capital space kwa kushirikiana na jukwaa la kuwezesha wanawake wajasiliamali, NDOTO HUB pamoja na Shule Direct ikiwa ni katika kuadhimisha wiki ya ubunifu nchini.