Dodoma FM

Miundombinu mibovu chanzo cha ugumu wa safari Kikuyu kaskazini

17 May 2021, 11:56 am

Na; Shani Nicolous

Wakazi wa kata ya Kikuyu kaskazini  jijini Dodoma wamelalamikia ubovu wa miundombinu ya barabara katika Kata hiyo hali inayosababisha ugumu wa  usafiri hasa msimu wa mvua wa mvua.

Wakizungumza na Dodoma fm wakazi hao wamesema kuwa ni muda mrefu shida hiyo ipo hasa katika Mtaa wa Kikuyu Magengeni barabara za mtaa huo hazina ubora hasa wanapotekeleza shughuli za kijamii.

Wameomba viongozi wao wawe na desturi ya kuweka mikutano mara kwa mara ili kusikiliza kero na changamoto za Kata na Mitaa yao kwa lengo la kuboresha miundombinu hiyo pamoja na mambo mengine.

Dodoma fm imezungumza na Diwani wa Kata ya Kikuyu Kaskazini Israel Mosses Mwansasu ambaye amesema kuwa  anafahamu changamoto hizo na tayari zipo katika utaratibu wa kufanyiwa kazi  hivyo anawataka wakazi wa Kata hiyo kutoa ushirikiano kwa viongozi katika kuleta maendeleo kama ilivyo kwa Kata nyingine zilizoendelea .

Viongozi wametakiwa kutambua wajibu wao na hasa kutatua changamoto na kuboresha baadhi ya mambo katika maeneo yao ili kuimarisha uaminifu kwa wananchi waliowachagua kwa ajili ya kuleta maendeleo ya nchi nzima.