Dodoma FM

Serikali yaahidi kusimamia sheria ya mtoto

21 May 2021, 12:43 pm

Na; Yussuph Hans

Katika kuhakikisha inawakomboa wanawake wanaobebeshwa mimba na kutelekezwa, Serikali imeahidi kusimamia ipasavyo sheria ya mtoto ya mwaka 2009 inayotoa maelekezo juu ya matunzo ya mtoto kwa wazazi wote wawili.

Hayo yamebainishwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anaeshughulikia maendeleo ya jamii Mh Mwanaidi Hamis, wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalum Mh.Neema Kichiki lililohoji nini mpango wa serikali kuwakomboa wanawake wanaobeba mzigo wa kugharamia matuzo ya watoto bila ya msaada wa baba.

Mh.Mwanaidi amesema ili kukabiliana na adha hiyo Serikali imeandaa sheria hiyo ili mzigo wa matunzo usiachwe kwa mzazi mmoja.

Ameongeza kuwa kwa wazazi ambao wametengana, mzazi wa kiume atawajibika kugharimia matunzo ya mtoto kulingana na kipato chake na mazingira anayoishi mtoto.

Katika hatua nyingine akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mh Latifa Hamis Juakali, Mh Mwanaidi amesema kuwa kwa kutambua umuhimu wa Bima ya Afya kwa kila mwananchi, serikali inakamilisha rasimu ya muswada kwa kutunga sheria ya bima kwa wote ambapo utawasilishwa Bungeni Ifikapo Mwezi Juni, 2021.

Bunge limeendelea leo Jijini Dodoma baada ya kusitisha vikao vyake jana kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Konde Khatib Said Haji (ACT-Wazalendo) aliyefariki katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa akipatiwa Matibabu.