Dodoma FM

NACTE yatakiwa kuandaa tathmini ya maonyesho ya vyuo vya ufundi

31 May 2021, 3:56 pm

Na; Rabiamen Shoo.

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka amelitaka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kuandaa mkutano wa tathimini ya maonyesho ya vyuo vya ufundi ili kuona tija ya maonyesho hayo.

Kauli hiyo aliitoa jana mara baada ya kutembelea mabanda ya Taasisi mbalimbali katika maonyesho ya pili ya elimu ya mafunzo na ufundi yaliyoandaliwa na NACTE kwa kushirikiana na Taasisi ya sekta binafsi (TPSF) yanayoendelea katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Mtaka amesema kuwa watafanya kikao cha kujadili namna pia ya kuwaendeleza wabunifu wa maonyesho hayo ili kazi zao ziwe na tija kiuchumi zaidi.

Pia ameitaka NACTE kuhakikishe mwakani mkoa unakuwa ni sehemu ya maandalizi ya mashindano haya,ili kusaidia kutangaza maonyesho hayo kikamilifu na kutoa hamasa kwa wananchi kuja kutembelea mabanda na kununua bidhaa zinazouzwa.

Mtaka amesema kuwa lengo la kufanya hivyo ni pamoja na kutaka kuboresha maonyesho hayo ya vyuo yaliyoandaliwa na NACTE ili yawe na msisimko zaidi kwa wananchi.

Pia Mhe.Mtaka amesema kuwa wao kama Mkoa wako tayari kushirikiana na waandaaji wa maonyesho ikiwemo kuwa na sehemu ambayo italea na kukuza wabunifu ambao watakuwa wamebuni teknolojia mbalimbali kupitia kwenye maonyesho husika.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa NACTE Dkt.Adolf Rutayuga amesema kuwa wao kama NACTE watayafanyia kazi ushauri na maoni yote aliyoyatoa ili kuleta tija zaidi katika maonyesho hayo mwakani.