Dodoma FM

Asilimia moja ya pato la Taifa yapotea kila mwaka kufuatia athari za mabadiliko ya Tabianchi

4 June 2021, 1:06 pm

Na;Mindi Joseph .

Asilimia 1 ya pato la Taifa inatajwa kupotea kila mwaka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi huku ikikadiriwa watu milioni 1.6 wanaoishi ukanda wa pwani watakabiliwa na changamoto ya athari za mabadiliko ya tabia nchi ifikapo mwaka 2030.

Akizungumza katika, uzinduzi wa  Mpango Mkakati wa Taifa wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi mwaka 2021 hadi 2026 Waziri wa Nchi , Ofisi ya Rais, Muungano na Mazingira Seleman Jafo amesema inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2030 wastani wa asilimia 2 ya pato la taifa itapotea.

Taswira ya habari imezungumza na Erneus Kaijage Mtaalam wa utafiti na sera kutoka taasisi ya Climate Action Network Tanzania amesema wanaendelea kujenga hoja na kuonyesha uhalisia kupitia utafiti wanaoufanya ili kushinikiza kuwepo kwa sera maalum itakayosaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake Abbas Kitogo Mtaalam wa miradi kutoka shirika la umoja wa mataifa la maendeleo UNDP amesema wanaendelea kushirikiana na serikali katika utekelezaji wa mkakati huo ili kujenga uelewa kwa jamii kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kuathiri sekta mbalimbali.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Shirika la CARE International Tanzania Bi.Haika Mtui amesema asilimia 65 ya wananchi wanategemea kilimo hivyo wataendelea kushirikiana na serikali ili kuboresha maisha ya wananchi.

Mabadiliko ya tabia nchi ni suala mtambuka ambalo linahitaji jitihada mbalimbali za wadau na jamii kwa ujumla ili kupunguza viashiria vinavyosababishia kuwepo mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia nishati mbadala ili kupunguza gesi ukaa ambazo zimekuwa chanzo kikubwa cha ongezeko la joto Duniani.