Dodoma FM

Finland kushirikiana na Tanzania kuboresha ustawi wa maendeleo ya jamii

4 June 2021, 12:55 pm

Na; Mariam Matundu.

Serikali ya Finland imedhamiria kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha kuwa Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii wanawezeshwa katika utekelezaji wa shughuli zao za uboreshaji wa huduma kwa jamii hususani uwezeshwaji wanawake kiuchumi.

Hayo yamebainika mkoani hapa wakati wa mazungumzo kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt John Jingu na Mkuu wa Ushirikiano wa Ubalozi wa Finland hapa nchini Dkt Timo Voipio yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara Jijini Dodoma.

Katika mazungumzo hayo Mkuu wa Ushirikiano wa Ubalozi wa Finland hapa nchini Dkt Timo Voipio amemuhakikishia Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt John Jingu kuwa Finland itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha Maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii wanawezeshwa ipasavyo ili kuhakikisha huduma za Jamii zinaboreshwa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya-Idara ya Maendeleo ya Jamii Dkt. Jingu amesema kuwa Wizara imeweka kipaumbele mkakati wa kuwawezesha Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii kwa kuwawezesha vifaa vya kazi vikiwemo usafiri na vifaa vya kieletroniki ili kuwezesha ufanisi wa majukumu yao.

Naye Kamishna wa Ustawi wa Jamii nchini Dkt Naftali Ng’ondi amesema kuwa Serikali inatumia mbinu mbalimbali katika kuwezesha mikakati iliyowekwa ya kuwainua wanawake kiuchumi ikiwa ni pamoja na Sekta zingine za maendeleo ya Jamii kuhusishwa katika utekelezaji wa mikakati hiyo.