Huheso FM

MASHARTI YA MILA ZA JADI CHANZO CHA MAGONJWA YA MILIPUKO MIGODINI

March 24, 2021, 10:31 am

Mgodi wa Mwime, Kahama.

IMEELEZWA kwamba mila na desturi za jadi, zinazoabudiwa na baadhi ya wachimbaji wadogo,zimekuwa ni miongoni mwa vyanzo vinavyochangia kuibuka kwa magonjwa ya milipuko kipindi cha masika katika maeneo ya migodi.

Hayo yalielezwa na Katibu wa Idara ya Afya na Mazingira, katika Mgodi wa madini ya dhahabu wa Mwime Two,Veronica Paul,kwa kubainisha kwamba kuna baadhi ya wachimbaji madini ambao hawana desturi ya kujisaidia haja kubwa na ndogo katika vyoo.

Veronica alisema baadhi ya watu wanaofika kufanya shughuli za uchimbaji huamini mafanikio ya katika shughuli hiyo hupatikana kwa kuamini kufanya vutendo vya jadi ambavyo huelekezwa kutofanya vitendo Fulani  ikiwemo kujisaidia ndani ya vyoo,kusudi wapate mafanikio.

Alisema utamaduni huo huwafanya kuwa na desturi ya kujisaidia vichakani pasipo kujali kuwa tabia hiyo inaathiri afya zao hasa kipindi cha masika ambapo kinyesi wanachokitoa na kutokihifadhi eneo husika kinaweza kuwasababishia maradhi ya milipuko.

“..tumewahi kuwakamata watu kadhaa wakijisaidia vichakani,wakadai ndio maelekezo waliyopatiwa wakati wakiagwa na bibi kuja kutafuta mali,kuwa ni marufuku kujisaidia ndani ya choo,”alisema bi Veronika.

Hata hivyo alisema wamekuwa na dhamira kubwa ya kutoa elimu ya usafi na mazingira kwa wachimbaji hao lakini kikwazo wanachokutana nacho ni wachimbaji hao kutokuwa tayari kuhudhuria mafunzo kwa madai yanawacheleweshea muda wa kutafuta mali.

Kwa upande wake Michael Kazimiri, mchimbaji mdogo katika machimbo ya Mwime, alisema kila mchimbaji anayefika katika mgodi huo huamini imani za jadi kuwa ndizo zitamletea mafanikio,hivyo ni budi watekeleze masharti wanayopewa na wataalamu wa mila kabla hawajafika migodini.

Na Misoji Masumbuko.