Huheso FM

Mwenyekiti wa kijiji halmashauri ya Ushetu asakwa na polisi kwa mauaji

April 21, 2021, 5:17 pm

Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linamsaka Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ikindika Kata ya Ushetu Wilaya ya Kipolisi Ushetu, Andrew Adam kwa tuhuma za mauaji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba amesema tukio hilo lilitokea Aprili 18 saa 4 usiku katika Kitongoji cha Ikindika, Kijiji cha Kidana, Kata ya Ushetu, Tarafa ya Dakama ambapo mtuhumiwa alimuua Daud Lubambula (49) kwa kumpiga chupa kichwani na kwenye mkono wa kulia.

Baada ya kipigo hicho, Daud alivuja damu nyingi na kupoteza maisha wakati akipatiwa matibabu katika kituo cha afya Ushetu.

Kamanda Magiligimba ametaja chanzo cha tukio hilo kuwa ni ugomvi uliotokana na ulevi kati ya marehemu na mtuhumiwa wakiwa kwenye kilabu cha pombe za kienyeji.

Hata hivyo Kamanda Magiligimba ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kufanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.

MWISHO