Jamii FM

IGP Sirro awahakikishia usalama wana Mtwara

22 November 2020, 13:45 pm

Mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP Simon Sirro akizungumza na wananchi wa kijiji cha kitaya halmashauri ya mji Nnyamba mkoani Mtwara, alipofanya ziara ya kikazi ya kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia unaimarika.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Simon Sirro amesema Jeshi la Polisi litachukua muda mfupi kukabiliana na uhalifu unaoendelea katika Mkoa wa Mtwara, kama ilivyofanya katika kukabiliana na mauaji ya raia katika Wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga mkoani Pwani.

IGP Sirro amesema hayo leo Novemba 22, 2020 wakati akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Kitaya mkoani Mtwara, ambapo ameahidi kuwa tatizo hilo halitachukua muda mrefu kwani vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kutokomeza uhalifu huo ,pia waliohusika na matukio ya utesaji raia na uharibifu wa mali zao wanachukuliwa hatua.

Wananchi wetu wamepata shida na waliofanya shida lazima washughulikiwe kwa mujibu wa sheria zetu kwa kushirikiana na Msumbiji sababu wana taarifa watu wanaotoka huko kuja kufanya Tanzania,amesema IGP Sirro.

 IGP Sirro ameongeza kuwa,Kimsingi ni kwamba, tumejipanga vizuri wananchi wetu waendelee kurudi kwenye yale maeneo waliyokimbia kule mpakani (mpakani mwa Tanzania na Msumbiji), tumeshajiimarisha, tutahakikisha hili tatizo litachukua muda mfupi kama ilivyokua kwenye tatizo la Kibiti na Ikwiriri ilivyochukua muda mfupi. Hawa wahalifu tutawashughulikia huko huko waliko”.

Lakini pia wananchi wa Kitaya na Nachenjele wamelipongeza jeshi la polisi kwa kuimalisha ulinzi na kufanya wananchi kurejea kwenye makazi yao, huku wakisisitiza jeshi la kuendelea kuimalisha ulinzi ili wanakijiji waweze kurudi katika shughuli za kilimo ,kwani ndio kazi pekee wanayoitegemea kuingiza kipato na kuendeleza maisha.

Taarifa hii inakuja siku moja baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Msumbiji Bernadino Rafael kufanya mkutano wa kupanga namna ya kuimalisha usalama kati ya Tanzania na Msumbiji katika ukumbi wa Naf Beach Hotel Mkoani Mtwara.

Sauti ya IGP Sirro Akizungumza na wananchi