Jamii FM

Umeme kumfikia kila mwananchi Tanzania nzima-Naibu waziri Nishati

4 July 2021, 16:59 pm

Na Gregory Millanzi

NAIBU Waziri wa Nishati Stephen Byabato amesema, Serikali itahakikisha kuwa, Nishati ya Umeme inamfikia kila mwananchi kupitia njia mbalimbali ili maendeleo ya Viwanda yaweze kuonekana kwa uhasilia.

NAIBU Waziri wa Nishati Stephen Byabato

Hayo yameelezwa leo na Naibu Waziri huyo wa Nishati wakati wakiwa kwenye Ziara ya kikazi mkoani Mtwara ambapo amepata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo kituo cha kufua umeme mkoani humo (Power Plant) pamoja na kiwanda cha Kuchakata Gesi Asilia kilichopo Madimba.

NAIBU Waziri wa Nishati Stephen Byabato akipata ufafanuzi kutoka kwa wahandisi wa Umeme

Lengo la ziara hiyo ni kukagua na kujionea namna ambavyo utekelezaji wa Nishati hiyo unavyoendelea Mkoani humo na kisha kuweza kuongeza ushauri na maelekezo ambayo yataleta uboreshaji wa kazi.

Moja ya mitambo ya kuzalisha umeme

Amesema Gesi ambayo inatumika kwa sasa nchini inatoka Mtwara na Lindi hivyo eneo hilo ni eneo la kimkakati kwa Serikali kwani wanalipenda na kuliheshimu ambapo Gesi kwa sasa ndio chanzo kikubwa na kipaumbele cha Serikali.

Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme (Tanesco) Mkoani Mtwara Mhandisi Bariki Ringo katika taarifa yake amesema kuwa hali ya upatikanaji wa wa Umeme kwa sasa imeimarika mkoani humo ikilinganishwa na kipindi cha mwaka mmoja uliyopita kwenye maeneo yote ya mkoa huo zikiachwa Wilaya za Masasi na Nanyumbu ambako bado kuna baadhi ya changamoto ambazo zinaendelea kufanyika kazi.

Hata hivyo mkoa huo una Vijiji 795 Kati ya hivyo Vijiji 406 ndiyo nyenye umeme na 386 havijapata Nishati hiyo ambapo Serikali imetenga Bilioni 60 ili kupekeleka umeme kwenye Vijiji 281 kupitia mpango wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili.

Kwa upande wake Meneja wa kituo cha kufua umeme Tanesco Mkoani humo (Power Plant) Mhandisi Didas Maleko amesema uwezo wa kituo hicho unakidhi mahitaji yote katika Mkoa wa Mtwara na Lindi na kituo kinahudumia Wilaya zote za Mtwara isipokuwa Wilaya ya Nanyumbu na Wilaya zote za Lindi isipokuwa Wilaya ya Kilwa na Lindi Mjini ambapo mahitaji ya juu ya Umeme yalipofikia kwa eneo la mkoa wa Mtwara ni megawati 18.