MIMBA ZA UTOTONI
Kahama FM

Mbaroni kwa kumpa Mimba bintiwa Darasa la nne.

March 31, 2021, 8:25 am

Jeshi la polisi mkoani Kagera linamshikilia Kusekwa Madaha (27) mkazi wa kijiji cha Murongo wilayani Kyerwa kwa tuhuma ya kumpa mimba mwanafunzi wa darasa la nne ambaye jina lake na la shule, vimehifadhiwa.

Kamanda wa polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi amesema kuwa mwanafunzi huyo aligunduliwa na mwalimu mkuu wa shule hiyo kuwa ana ujauzito wa miezi minne.

“Baada ya kugundulika kuwa ni mjamzito alihojiwa na kumtaja mtuhumiwa kuwa ndiye alimpa ujauzito huo, tunamshikilia na uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani” amesema.

Amesema kufuatia kuanza kujitokeza kwa matukio ya kuwabaka na kuwapa mimba wanafunzi, jeshi hilo litawasaka na kuwakamata wale wote watakaobainika kuwapa mimba wanafunzi.

“Nitumie nafasi hii kutoa onyo kwa watu hao kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, mtu anayewinda na kuharibu maisha ya wanafunzi ni sawa na kujihusisha na dawa za kulevya, nguvu tutakayoitumia kuwasaka ni sawa na ile tunayotumia kuwasaka watuhumiwa wa dawa hizo” amesema.