SHINYANGA
Kahama FM

Wachenjuaji wa dhahabu wajenga kituo cha Polisi

April 2, 2021, 7:36 am

MKUU wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko ameeleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa kituo cha Polisi kilichopo kwenye machimbo ya Dhahabu Mwakitolyo wilayani Shinyanga, ambacho kitasaidia kuimarisha ulinzi na usalama katika eneo hilo.

Picha ya pamoja kati ya wachenjuaji wa Dhahabu na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga.

Mboneko amebainisha hayo leo alipofanya ziara kwenye machimbo hayo kukagua ujenzi wa kituo hicho ambacho kimejengwa kwa nguvu za umoja wa wachenjuaji wa madini ya dhahabu wa Mwakitolyo (UWADHAMWA) kwa kuchangishana pesa, kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama kwenye eneo hilo.

Amesema anapongeza sana umoja huo wa wachenjuaji wa madini ya dhahabu kwa kuitikia agizo lake na kuamua kuanza ujenzi wa kituo cha Polisi kwenye machimbo hayo, ambacho ni muhimu sana kutokana na shughuli zao za uchimbaji wa madini, kwa kuwahakikishia amani inatawala kwenye maeneo hayo na hakuna uvunjifu wa amani tena.

Aidha amesema kukamilika pia kwa ujenzi huo wa kituo cha Polisi, kutatoa fursa kwa wafanyabishara na wawekezaji kuwekeza kwenye mgodi huo wa Mwakitolyo, pamoja na Taasisi za kifedha kusogeza huduma kwenye maeneo hayo, wakiwamo TRA kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato.

Naye Mkuu wa Polisi Wilaya ya Shinyanga, John Kafumu, amesema kituo hicho cha Polisi kitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya uharifu kwenye maeneo hayo yakiwamo ukatwaji wa mapanga, sababu Askari Polisi watakuwa doria masaa 24 ili kuhakikisha amani inatawala.

Aidha Mwenyekiti wa Wachimbaji wa Madini ya Dhahabu Mwakitolyo, Aphonce Paulo, amesema walikuwa na hamu sana ya kupatiwa kituo cha Polisi kwenye maeneo hayo kutokana na usalama kuwa hafifu, na ndio maana wakahamasishana kuanzisha ujenzi wa kituo hicho ili wawe salama na mali zao.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Shinyanga, John Kafumu, akizungumza mara baada ya kumaliza ukaguzi ujenzi wa kituo cha Polisi Mwakitolyo wilayani Shinyanga.

Kwa upande wake Katibu Msaidizi wa Umoja huo, Elisha Rugwisha, akisoma taarifa ya ujenzi huo wa kituo cha Polisi amesema ulianza Februari mwaka huu, na sasa upo katika hatua ya Renta, na unatarajiwa kukamilika mwezi huu kwa zaidi ya gharama ya Sh. Milioni 30.