UBAKAJI
Kahama FM

MLINZI AMUUA MKEWE AKITUMIA DAWA ZA ARV KWA KUJIFICHA.

May 7, 2021, 7:25 pm

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba

Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga linamshikilia Peter Elias (29) mlinzi na mkazi wa Ndembezi Mjini Shinyanga kwa kosa la kumuua mke wake Pili Luhende akimtuhumu kutumia Dawa za Kufubaza Makali ya Virusi vya Ukimwi ‘ARV’ kwa kificho.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Ijumaa Mei 7,2021 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba tukio hilo limetokea Mei 3,2021 majira ya saa nne na nusu usiku katika mtaa wa Dome, Kata ya Ndembezi, Manispaa ya Shinyanga.
“Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga tulipokea taarifa kuwa Pili Luhende, aliuawa na Peter Elias (29), mlinzi na mkazi wa Ndembezi ambaye ni mume wake baada ya kumpiga. Baada ya taarifa hiyo mtuhumiwa alikamatwa na kuhojiwa ambapo tarehe 06/05/2021 alionyesha alipoutelekeza mwili wa marehemu maeneo ya Mwagala darajani”,ameeleza Kamanda Magiligimba.
Pia alibainisha kuwa alimpiga kwa kutumia ngumi na chanzo kikiwa ni mtuhumiwa kumbaini mkewe anatumia dawa za HIV yaani ARV kwa kificho hivyo ikamtia hasira na wamekuwa na ugomvi wa mara kwa mara kuhusiana na hilo”,ameongeza .
Amesema mwili wa marehemu umekutwa ukiwa umeharibika na umekabidhiwa kwa ndugu kwa taratibu za mazishi na kwamba mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Kamanda Magiligimba anatoa wito kwa wanandoa/wenzi kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake wapeleke malalamiko yao kwenye madawati ya jinsia na watoto yaliyopo vituo vya polisi ukatili wa kijinsia polisi pamoja na ustawi wa jamii ili kupata suluhisho la migogoro yao.