Kahama FM

Kaya masikini kunufaika na mradi wa TASAF Kahama.

July 7, 2021, 10:55 am

Mkuu wa wilaya ya Kahama FESTO KISWAGA

Serikali wilayani Kahama mkoani Shinyanga imewataka viongozi, wawezeshaji na watendaji kutoa elimu kwa kaya masikini zinazopatiwa ruzuku ili fedha wanazopata waweze kijikimu na kuongeza kipato chao, kwa kuanzisha miradi itakayowapatia kipato cha kudumu.

Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Kahama FESTO KISWAGA wakati akifungua kikao kazi cha kujenga uelewa kuhusu sehemu  ya pili awamu ya tatu     ya  TASAF kwa viongozi, watendaji na wawezeshaji ambapo amesema kuwa kipindi hiki kaya masikini zinapaswa kupatiwa elimu kabla ya kupatiwa fedha hizo ili ziwe na tija kwao.

Naye mwakilishi wa mkurugenzi mtendaji wa TASAF nchini MERCY MANDAWE amesema kuwa katika kipindi cha awamu ya kwanza, kuna maeneo ambayo hayakufikiwa, ambapo kwa kipindi cha awamu ya tatu yatafikiwa maeneo yote yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa halmashauri ya msalala FLORA SAGASA na Meya wa manispaa ya Kahama YAHAYA RAMADHANI wamesema kuwa TASAF wanapaswa kuangalia wenye sifa za kupata ruzuku kwa kuzingatia taratibu  na kanuni za utoaji wa ruzuku hiyo kwa kuwanufaisha walenga.

wakati huohuo, mtaratibu wa kunusuru kaya masikini (TASAF) Manispaa ya Kahama LEONARD NCHINJAI amesema kuwa kwa manispaa ya Kahama ruzuku hiyo itakwenda kuwanufaisha katika maeneo ambayo kwa awamu zilizopita hawakupata, na awamu hii zitapata kaya zote ambazo zina sifa  ya kupata ruzuku hiyo.

Hata hivyo, TASAF katika tathimini ya utekelezaji wa kipindi cha awamu ya tatu imeonesha kuwa  mradi huo umechangia katika kufikiwa kwa azma ya serikali ya kupunguza umasikini nchini.