Karagwe FM

Watuhumiwa wa wizi wafyekewa Migomba na kubomolewa Nyumba.

18 May 2021, 8:59 pm

Wananachi wenye hasira kali katika kijiji cha Rukole kata Ihanda wilaya ya Karagwe mkoani Kagera wamevamia na kubomoa nyumba pamoja kufyeka migomba ya wananchi wa kitongoji cha Kalalo wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu kijijini humo.

Migomba iliyofyekwa

Akizungumuza katika eneo la tukio mwenyekiti wa kitongoji cha Kalalo kijiji cha Rukole kata ya Ihanda mahali lilikotokea tukio hilo Godfrey Fabian amesema kuwa tukio hilo limetokea majira ya saa tisa za usiku mei 18 mwaka huu ambapo wananchi wenye hasira kali wamebomoa nyumba pamoja na kufyeka mashamba ya migomba.

Bwana Fabian amesema kuwa chanzo cha tukio hilo ni wananchi kuchukizwa na kitendo cha watuhumiwa waliotajwa kwa majina ya Joansen Anatory na Yaunde Onesmo ambao awali walikuwa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi wilaya Karagwe kwa tuhuma za vitendo vya uhalifu na kisha watuhumiwa hao kurudi mtaani na kuwatambia wananchi kuwa hawana namna ya kuwadhibiti.

Mtendaji wa kijiji cha Rukole Bwana Godfrey Nyeme amewasiliana na Jeshi la Polisi wilaya Karagwe ambapo muda mfupi baada ya Jeshi hilo kufika katika eneo la tukio wamefanikiwa kuwatuliza wananchi na kunusuru maisha ya Bwana Joansen Anatory ambaye alisalia katika eneo la tukio huku mwenzake Yaunde Onesmo akitokomea kusikojulikana.

Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi wilaya ya Karagwe Henry Benard Makwasa amethibitisha kutokea kwa tukio na kuwataka wananchi wa wilaya Karagwe kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi.

Godfrey Fabian – Mwenyekiti wa Eneo la tukio