Mazingira FM

Anusurika kifo baada ya kushambuliwa na Nyati

21 June 2021, 9:26 am

By Edward Lucas

Magesa Magori mkazi wa Tamau

Kijana aitwaye Magesa Magori (21) mkazi wa Mtaa wa Tamau, Kata ya Nyatwali Halmashauri ya Mji wa Bunda Mkoani Mara anusurika kifo baada ya kuvamiwa na mnyama nyati wakati akiwa anachunga ng’ombe maeneo ya Tamau.

Akisimulia tukio hilo amesema, ilikuwa ni siku ya Ijumaa 11 June 2021 majira ya mchana akiwa na ndugu yake maeneo ya Tamau wanachunga ng’ombe mara ghafla walisikia kishindo cha wanyama wakikurupuka kukimbia ndipo walipotambua kuwa lilikuwa ni kundi la nyati.

Amesema baada ya muda wakiwa karibu na eneo hilo ndipo walipobaini kuwa kuna nyati mmoja alikuwa amesalia na ghafla alianza kuwakimbiza na kufanikiwa kumfikia kijana huyo wakati akijitahidi kuingia kwenye kichaka ndipo alipoanza kuushambulia mguu wa kushoto uliokuwa umebaki kwa nje wakati sehemu nyingine ya mwili ikiwa ndani ya kichaka

Sehemu ya majeraha aliyoyapata Magesa katika mguu wake wa kushoto baada ya kupokea matibabu kutoka hospitali ya DDH Bunda na kuruhusiwa kurudi nyumbani

“Baada ya kishindo hicho nikajua ‘yameenda’ kumbe moja likawa limejificha, nikakaribiana nalo jirani tu ndio likanishitua yaani ile kukimbia tu kuingia kwenye kichaka likaanza kunichomachoma” Magesa alisimulia na kuongeza kuwa
“Nikaanza kupiga yowe ndio mwenzangu akaja, akanivuta pembeni kidogo ndio akaenda mwaloni akawaambia wakanifata wakanipeleka hospitali” Magesa alisimulia

Kwa upande wake shuhuda wa tukio hilo Werema Magori ambaye ni nduguye amesema baada ya kukimbia yeye akiwa ametangulia mbele ghafla alianza kusikia sauti ya nduguye akilia na kuomba msaada ndipo aliporudi na kukuta nyati huyo akiwa anaondoka huku mwenzie akiwa amelala kichakani damu zinatiririka katika mguu wake wa kushoto.

Werema ameongeza kuwa baada ya kuona hali hiyo alipiga kelele kuomba msaada pasipo mafanikio ndipo aliposogea karibu na watu waliokuwa maeneo ya ziwani kuwaomba msaada ambapo walifika na kumpeleka hospital ya DDH mjini Bunda.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Tamau, Asafu Ernest Owiti akifanya mazungumzo na Mtangazaji wa Radio Mazingira kuhusu tukio hilo na hali ya usalama katika eneo hilo kufuatia uvamizi wa wanyama waharibifu

Mazingira Fm imezungumza na Mwenyekiti wa mtaa wa Tamau, Asafu Ernest Owiti kuhusu tukio hili ambapo amekiri kuwa alipokea taarifa za tukio hilo na kusema kuwa licha ya kuwa maeneo hayo yamekuwa wakipata matukio mbalimbali ya wanyama waharibifu kama tembo, kiboko na mamba hawajawahi kupata tukio la watu kuvamiwa na mnyama aina ya nyati kwa hivi karibuni.

“Taarifa hizi nimezipata siku ya Tarehe 12 siku ya Jumamosi Asubuhi, kwa maana siku ya tukio (11 June 2021) nilikuwa kwenye kikao cha WDC baada ya kupata taarifa hizi kweli nilifika nakumuona kijana aliyejeruhiwa na nyati” Asafu alisema

“Nadhani kwa masuala ya hao wanyama sasa imekuwa imezidi kwasababu wanyama tuliokuwa tumewazoea sana wanafanya matukio hapa ni tembo ambao wanaharibu mashamba ya watu pia niseme na matukio ambayo yamezoeleka sana ni mimba kwa hili la nyati ndio tukio la kwanza”

Asafu aliongeza kuwa katika maeneo hayo ambayo kijana huyo anadai kushambuliwa na Nyati huyo yanajulikana kwa jina la ‘magwata’ yametengwa maalumu kwa ajili ya shughuli za malisho ya mifugo ya wananchi

Aidha, Asafu amewataka wananchi wa kuchukua tahadhali mbalimbali dhidi ya wanyama waharibifu hususani kwa mnyama nyati ambao wametajwa kuonekana katika maeneo hayo.

Diwani kata ya Nyatwali, Mh Malongo Mashimo akifanya mahojiano na Mtangazaji wa Radio Mazingira kuhusu matukio ya wanyamapori kuvamia makazi ya watu na kusababisha uharibifu, kujeruhi na wakati mwingine vifo.

Katika hatua nyingine Mazingira Fm imezungumza na Diwani wa eneo hilo la Nyatwali, Malongo Mashimo ambapo kwa upande wake amesema kuwa matukio ya wanyama waharibifu kuvamia makazi ya watu na kuharibu mali za watu, kujeruhi na kuua watu yamekuwa yakirudisha nyuma maendeleo ya watu na kata kwa ujumla

Matukio ya wanyama waharibifu kujeruhiwa, kuawa na kuharibu mali za watu hususani mazao yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara katika maeneo mengi Wilaya ya Bunda.