Radio Fadhila

Gwiji Wa Soka Diego Maradona Afariki Dunia

26 November 2020, 9:48 AM

Nyota wa Soka raia wa Argentina, Diego Maradona amefariki Dunia akiwa na umri wa miaka 60 kwa mshtuko wa moyo,  Novemba 25, 2020, ikiwa ni wiki mbili tu baada ya kuruhusiwa kutoka Hospitali alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya oparesheni ya ubongo.

Maradona atakumbukwa kwa umahili wake kwenye soka hasa alivyoisaidia timu yake ya Taifa ya Argentina kutwaa Kombe la Dunia mwaka 1986. Amewahi kuchezea vilabu vikubwa duniani kama Boca Juniors, Napoli na Barcelona na kuwa tishio uwanjani huku akijikusanyia mamilioni ya mashabiki kila kona ya dunia.

Maradona aliifungia Argentina magoli 34 katika michezo 91, akishiriki michuano minne ya Kombe la Dunia.

Aliliongoza Taifa lake katika fainali ya Kombe la Dunia la mwaka 1990 nchini Italia, ambapo walifungwa na Ujerumani Magharibi.

Alikuwa tena nahodha wa taifa lake katika mashindano ya 1994 nchini Marekani lakini alirudishwa nyumbani baada ya kubainika alitumia dawa za kuongeza nguvu.

Wiki mbili zilizopita Maradona alilazwa hospitali kwa tatizo la damu kuvuja kwenye ubongo wake . Tatizo hilo madaktari walipambana nalo na kufanikiwa kuliondoa na kumruhusu arudi nyumbani.

Katika miaka yake ya mwisho ya uchezaji aligubikwa na utumiaji wa dawa za kusisimua misuli pamoja na dawa za kulevya.