Radio Fadhila

SERIKALI wilayani Masasi mkoani Mtwara imewataka madiwani wa Halmashauri zilizopo wilayani humo kutoendeleza makundi ya kisiasa

17 December 2020, 11:12 AM

SERIKALI wilayani Masasi mkoani Mtwara imewataka madiwani wa Halmashauri zilizopo wilayani humo kutoendeleza makundi ya kisiasa kwa kudhani kuwa kampeni za uchaguzi bado zinaendelea, badala yake wavunje makundi na kuwa kitu kimoja katika kupambana kwa ajili ya maendeleo ya wananchi waliowachagua.
Wilaya ya Masasi inaundwa na Halmashauri mbili, Halmashauri ya mji Masasi na Halmashauri ya wilaya ya Masasi.
Wito huo ulitolewa jana na katibu tawala wilaya ya Masasi, Mohammed Azizi( pichani) alipokuwa akifungua kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi, kikao hicho kiliketi kwa ajili ya Madiwani hao kuala kiapo rasmi ili waweze kuanza kutekeleza majukumu yao kisheria.
Katibu tawala huyo pia alitoa kauli kama hiyo juzi katika baraza la Madiwani wa Halmashauri ya mji Masasi.
Alisema kuwa wajibu wa madiwani ni kuwatumia wananchi kwa kuwasemea na kutafuta njia bora ya kutatua kero zao, hivyo madiwani wasitumie muda wao na nafasi zao kutengenezeana majungu pasipo na tija kwa wananchi wao.
Alisema si wakati wa kuendeleza makundi uchaguzi umekwisha na sasa ni wakati wa kufanya kazi za kuleta maendeleo kwa manufaa ya Masasi na taifa kwa ujumla.