Radio Fadhila

Rais Mwinyi Asamehe Wafungwa 49

12 January 2021, 3:18 AM

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa msamaha kwa wanafunzi (wafungwa) Arobaini na Tisa (49) waliokuwa wakitumikia Vyuo vya Mafunzo vya Unguja na Pemba ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za Sherehe za miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Dk. Mwinyi ametoa msamaha huo kwa mujibu wa kifungu cha 59 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kinachompa mamlaka ya kutoa msamaha kwa wafungwa waliofungwa gerezani.

Kutokana na msamaha huo, Dk. Mwinyi ameamuru kuwa kifungo kilichobaki cha wanafunzi (wafungwa) hao walionufaika na msamaha katika vyuo vya Mafunzo vya Unguja na Pemba kuwa kipindi hicho chote kinafutwa na waachiwe huru kuanzia Januari 11.2021.